Thursday, July 19, 2012

250 wazama Zanzibar.Wengi wahofiwa kufa wakiwamo raia wa kigeni

KWA mara nyingine Kisiwa cha Zanzibar kimekumbwa na msiba mzito kutokana na kuzama kwa meli ya mv Skagit, mali ya Kampuni ya Seagull, iliyokuwa ikisafiri kutoka jijini Dar es Salaam ikiwa na abiria wanaokadiriwa kuwa kati ya 200 hadi 250 pamoja na mizigo kuelekea Unguja, visiwani Zanzibar jana saa saba mchana.
Hii ni ajali nyingine mbaya kutokea visiwani humo ambapo Septemba mwaka jana, meli ya Spice Islander inayomilikiwa na kampuni hiyo ilizama ikiwa safarini kuelekea Pemba ikitokea Bandari ya Malindi, Unguja na watu zaidi ya 240 kupoteza maisha na wengine 619 kuokolewa.
Chanzo halisi cha kuzama kwa meli hiyo kusini mwa Kisiwa cha Chumbe bado hakijafahamika wala idadi kamili ya watu waliopoteza maisha nayo haijajulikana, ingawa taarifa za awali zinasema hali mbaya ya hewa baharini ilichangia ajali hiyo.
Hadi tunakwenda mitamboni usiku, taarifa zilizotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia kwa Kaimu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mwinyi Haji Makame, zilisema kuwa maiti za watu 15 zilikuwa zimepatikana, wakiwamo watoto wanne na raia mmoja wa Kizungu, huku 124 wakiokolewa.
“Miili yote inapelekwa uwanja wa Maitara kwa ajili ya kutambuliwa na ndugu zao, lakini wako baadhi ya abiria zaidi ya 124 wameokolewa wakiwamo raia 13 wa Kizungu na majeruhi wote wamelazwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja,” alisema Makame.
Aliongeza kuwa shughuli za uokoaji zinaendelea kufanywa na vyombo vyote vya usalama licha ya hali ya mawimbi kuwa mbaya kiasi cha boti za uokozi kupata taabu ya kuwafikia abairia hao.
Naye msemaji wa Jeshi la Polisi, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Advera Senso, alisema meli hiyo inakadiriwa kubeba abairia zaidi ya 200 wakiwamo watoto 31.
“Bado tunafuatilia zaidi na tunafanya jitihada za uokoaji kwa kutumia helikopta ya Polisi na taarifa nyingine zaidi tutatoa baadaye kadiri zinavyopatikana maana wote tunaelekea huko,” alisema.
Hata hivyo, taarifa zilizotufikia kutoka visiwani humo ni kwamba shughuli za uokoaji zinaendelea na boti zisizopungua nne zimekwisha kufika eneo la tukio kwa ajili ya kuwaokoa abiria hao.
Meli hiyo mara kwa mara imekuwa na matatizo ya kiufundi na kusababisha kupata hililafu ikiwa katikati ya safari baharini.
Mwezi Mei abiria zaidi ya 300 walinusurika kufa baada ya meli hiyo kushika moto ulioanzia kwenye injini wakati ikitokea Pemba kwenda Unguja.
Kipindi hicho taarifa zilisema meli ilikuwa ikitokea Bandari ya Mkoani na ilipokaribia eneo la Nungwi ilikwenda mwendo usio wa kawaida na kupoteza mwelekeo na kisha kuzima kabisa injini.
Bunge laahirishwa
Kutokana na ajali hiyo, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Baraza la Wawakilishi, yaliahirisha vikao vyao jana ili kutoa nafasi kwa baadhi ya viongozi kuelekea eneo la tukio.
Hata hivyo, mjini Dodoma, wabunge wa kambi ya upinzani walilazimika kutoka bungeni kwa nguvu baada ya Spika, Anne Makinda, kupuuza hoja ya Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF) ya kuomba Bunge lisitishe kikao chake kutokana na ajili hiyo, wakidai anapuuza masuala ya msingi.
Ilikuwa majira ya saa 11 wakati Bunge likianza awamu ya pili ya jioni ambapo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Emmanuel Nchimbi, alikuwa akijibu hoja za wabunge, ndipo Hamad aliomba mwongozo wa Spika wa Bunge akitaka bajeti ya wizara hiyo ipitishwe kwa mafungu ili wabunge waende kwenye tukio hilo.
Hamad alitumia kanuni ya 47 (3) inayosema kuwa hoja itatolewa na mbunge kwa kusimama mahali pake na kuomba idhini ya Spika kutoa hoja ya kuahirisha shughuli za Bunge kwa madhumuni ya kujadili jambo halisi la dharura na muhimu kwa umma.
Hata hivyo Spika Makinda alikataa kuahirisha shughuli za Bunge akisema kanuni hiyo inatumika vibaya, kwani ilitakiwa jambo hilo liwe limetokea eneo lililo karibu na Bunge.
Alisema watahitajika wabunge wawahi kutoa damu au msaada wowote wa haraka lakini kwakuwa limetokea Zanzibar, wabunge hawawezi kutoa msaada wowote kwa haraka, zaidi ya kupiga simu kujua kilichotokea.
“Nimeshawasiliana na waziri anayehusika na majanga na wamekubaliana kuwa awasiliane na wahusika waliopo kwenye eneo la tukio na kisha tutajua tutakavyojipanga,” alisema Makinda.
Baada ya kauli hiyo idadi kubwa ya wabunge bila kujali itikadi za vyama vyao waliamua kuondoka ndani ya ukumbi kuonyesha ishara ya kutokubaliana na uamuzi huo.
Wabunge hao waliamua kwenda katika Ukumbi wa Pius Msekwa huku wengi wakilia wakionyesha kuguswa na tukio hilo.
Wakiwa ndani ya Ukumbi wa Bunge, Hamad Rashid, aliwaambia wenzake kuwa alipata taarifa juu ya kuzama kwa meli hiyo na anafanya utaratibu wa kupata ndege ya serikali.
Alisema alijaribu kuwasiliana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, bila mafanikio kuwajulisha na kupanga utaratibu.
Alibainisha kuwa watachagua baadhi ya wabunge wa Bara na Visiwani pamoja na kuomba ndege ya serikali ili waende Zanzibar.
“Watu wamekufa Spika hataki kuahirisha Bunge, sisi hatukubali kuendeshwa na watu wasiojali utu,” alisema Hamad.
Hata hivyo, jitihada za Spika kutaka Bunge liendelee na hoja hiyo hazikufua dafu baada ya Waziri Nchimbi kuwasilisha hoja yake kumwomba akubali kuahirisha shughuli za Bunge kutokana na udharura wa kuzama kwa meli hiyo.
Dk. Nchimbi akitumia kanuni ya 58 (5) ambayo inasema endapo hoja imefikishwa bungeni, mtoa hoja anaweza kuiondoa hoja yake kwa kusimama mahali pake na kusema:  “Ninaomba ruhusa kuondoa hoja.”
Aidha Dk. Nchimbi alisema kuwa kutokana na Spika kumwelekeza yeye kuwasiliana na Kamishina wa Zanzibar, ilibainika kuwa hali ni mbaya na kamishna alimweleza kuwa yupo katika eneo la tukio, hivyo kwa muda aliofikiria kuwa angeweza kuwasilisha hoja hautoshi, hivyo kuomba kuondoa hoja hiyo.
Spika Makinda aliwauliza wabunge kama wanaafiki hoja hiyo kuondolewa na wabunge walikubaliana nayo na kisha akawataka wajumbe wa kamati ya uongozi kukutana ili kujadili jambo hilo na kuangalia njia sahihi za kuchukua.
Spika kung’olewa?
Baadhi ya wabunge wameanza kuwahamasisha wenzao kupiga kura ya kutokuwa na imani na Spika wa Bunge.
Wabunge hao walifikia hatua hiyo kwenye kikao cha dharura walichokifanya jana katika Ukumbi wa Pius Msekwa kwa lengo la kufanya maandalizi ya kwenda Zanzibar kuhudhuria msiba wa wenzao waliozama katika ajali meli ya Skagit.
Mbunge wa Mji Mkongwe, Muhammad Ibrahimu Sanya (CUF), alisema Spika Makinda hana utu ndiyo maana aligoma kuahirisha shughuli za Bunge ili kutoa nafasi ya watu kushiriki kwenye jambo hilo.
“Huyu Spika hatufai, yaani vifo vikitokea kwa watu wa Bara yeye ndiyo ataona kuna uzito…hapa alikufa Amina Chifupa tukaahirisha Bunge, sasa iweje wenzetu wamekufa kule Zanzibar yeye akatae kuahirisha shughuli za Bunge? Jamani tujipange kupiga kura za kutokuwa na imani naye, ameonyesha kushindwa kulihimili Bunge,” alisema.
Mbunge mwingine kutoka Zanzibar alisema hawaoni sababu ya kuendelea na mjadala wa bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa sababu wapiga kura wao ndio waliofariki dunia.
“Tuna raha gani ya kuendelea kujadili hotuba ya bajeti, huyu Spika tumedhihirisha hana uwezo wa kutuongoza, hatufai, waliokufa kule ni binadamu si paka wala wanyama,” alisema.