Tuesday, September 24, 2013

Waathiriwa wa shambulizi la Westgate



Ruhila aliolewa mwaka jana
Takriban watu 62 wameuawa kwenye mashambulizi ya kigaidi nchini Kenya dhidi ya jengo la kifahari lenye maduka zaidi ya themanini la Westgate.

Ruhila Adatia-Sood

Ruhila Adatia-Sood na mumewe Ketan Sood Ruhila Adatia-Sood walioana tu mwezi Januari mwaka jana.
Ruhila, alikuwa katika ghorofa ya juu ya duka la Westgate ambako alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wameandaa mashindano ya upishi kwa watoto.
Alikuwa ameolewa na Ketan Sood, aliyefanya kazi na shirika la USAid mjini Nairobi mwezi Januari mwaka 2012,na harusi yake ilitajwa kuwa harusi ya kiswahili ambayo ilisherehekewa kwa siku tatu.
Alikuwa mjamzito na mimba ya miezi sita alipofariki.
Kulingana na ripoti Adatia-Sood alikimbizwa hospitalini , lakini alifariki baada ya kuwasili kutokana na kuvuja damu nyingi.
Alisifika kote nchini kwa moyo wake mzuri wa kuwafanya watu kutabasamu daima.

Polisi wakikabiliana na wanamgambo hao waliokuwa wameteka jengo la Westgate
Kwenye ukurasa wake wa Twitter alijitaja kuwa mpenda chakula na mtu mwenye kufurahia michezo ya kusisimua.
Alisomea katika chuo kikuu cha Rhodes nchini Afrika Kusini , na dada zake watatu wamemtaja kama mtu mwenye ari kubwa maishani.
Pia alikuwa mtangazaji wa kituo cha redio cha East FM na pia alitangaza habari kwenye kituo cha televisheni ya Kiss.
Magaidi waliwarushia magurunedi Rahila na mtangazaji mwenzake pamoja na watoto waliokuwa ndani ya jengo hilo lakini Ruhila hakuponea. Mwenzake Kamal Kaur, pia mtangazaji wa redio alikuwa ameambatana na watoto wake ambao walifyatuliwa risasi ingawa ziliwakosa na kumgonga mtoto aliyekuwa karibu nao. Wao walijeruhiwa miguuni.
Kaur na wanawe walifanikiwa kukimbilia usalama wao.

Mbugua Mwangi and Rosemary Wahito

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta pia aliwapoteza jamaa zake katika shambulizi hilo. Mbugua Mwangi ni mpwa wa Kenyatta na alikuwa na mchumba wake Rosemary Wahito wakati waliposhambuliwa kwa risasi na kuuawa papo hapo.
Akihutubia taifa, Kenyatta alisema kuwa, "ninamuomba Mungu awape utulivu wakati sote tukikumbwa na msiba huu na ninajua mnachokihisi hasa ikiwa umempoteza jamaa wako katiakshambulizi hili baya.''
Kulingana na taarifa ya jarida la nchini Ireland, mamake Mwangi, Catherine Muigai Mwangi, ndio alikuwa tu amerejea kutoka Dublin ambako alikuwa balozi wa Kenya kwa miaka sita .
Dadake mkubwa Rais Kenyatta Christine Wambui Pratt pia alikuwa katika jengo hilo lakini alifanikiwa kunusuru maisya yake.

Mitul Shah


Mitul Sha alipenda sana soka
Mitul Shah Mitul Shah alikuwa mkuu wa timu ya soka ya kampuni yake ambayo inacheza katika divisheni ya pili.
Afisaa mkuu mtendaji wa mauzo katika kampuni ya Bidco, ambayo hutengeza mafuta ya kupikia, Mitul Shah alikuwa katika ghorofa ya juu zaidi ya jengo hilo.
"Alifariki akijaribu kuwaokoa watoto waliokuwa wamekwama ndani ya jengo hilo. Kwa marafiki wa Mitul, alifariki kama shujaa .
Rafiki zake wamemtaja kama shabiki sugu wa Manchester United.
Pia alikuwa mwenyekiti wa timu ya soka ya Bidco.

Joyti Kharmes Vaya na Maltiben Ramesh Vaya ambao ni wifi


Mazishi ya Joyti Kahrmes Vaya na Maltiben Ramesh Vaya
Joyti Kharmes Vaya alikuwa na umri wa miaka 37 mwenye watoto watatu, ambaye mumewe alifanya kazi katika benki ya Victoria Commercial bank.
Maltiben Ramesh Vaya alikuwa na miaka 41 , mama wa watoto wawili aliyefanya kazi katika Benki ya Baroda.
Wawili hao walikufa kutokana na majeraha waliyopata, kutoka na risasi

Kofi Awoonor

Raia wa Ghana mwenye umri wa miaka 78 malenga anayesifika sana. Anasifika nyumbani kwao kama mwandishi ambaye vitabu vyake vinatumiwa katika shule nyingi nchini Ghana.
Alikuwa mjini Nairobi kushiriki hafla ya Storymoja na alitarajiwa kutumbuiza watu siku ya Jumamosi.
Alisifika kwa nyimbo na mashairi yake mapema miaka ya sitini.
Miaka ya sabini alifunza katika baadhi ya vyuo vikuu nchini Marekani na kurejea Ghana mwaka 1975 kuchukua wadhifa wa mwalimu wa lugha ya kiingereza katika chuo kikuu cha Cape Coast.
Katika muda wa miezi kadhaa, alikamatwa na kuzuiliwa kwa madai ya njama ya uhaini wakati wa utawala wa kijeshi wa Kanali Ignatius Acheampong.
Mwanawe Awoonor alikuwa naye wakati wa shambulii hilo mjini Nairobi na alipigwa risasi mkononi wakati wa shambulizi hilo.


Chanzo: BBC SWAHILI

Vikosi vya Kenya 'vimedhibiti' Westgate


Moshi mkubwa ulioonekana ukifuka kutoka katika jengo la Westgate Jumatatu jioni Hatimaye vikosi vya usalama nchini Kenya vinasema vimelidhibiti jengo zima la Westgate mjini Nairobi, ikiwa ni zaidi ya siku tatu baada ya jengo hilo kuvamiwa na wanamgambo.

Milipuko ikifuatiwa na milio ya risasi imesikika kutoka ndani ya jengo hilo asubuhi ya leo huku duru zikisema kuwa vikosi vya usalama vinaelekea kukamilisha operesheni hiyo.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, magaidi sita waliokuwa wamesalia wameuawa huku wengine watatu wakiuawa hapo jana.

Serikali imesema zaidi ya watu 60 wameuawa na wengine zaidi ya 170 kujeruhiwa katika shambulio hilo ambalo Al shabaab imekiri kulitekeleza.

Wizara ya mambo ya ndani imesema wanajeshi wanaendelea kulisaka jengo zima la Westgate kutoka orofa moja hadi nyengine kuhakikisha kwamba hakuna mateka aliyesalia

Wakati huohuo, waziri wa mambo ya nje amesema kuwa wawili kati ya wanamgambo watatu waliofanya shambulii hilo ni raia wa Marekani pamoja na mwanamke muingereza.

Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televisheni nchini Marekani, Amina Mohamed alisema kuwa wamarekani walikuwa kati ya umri wa miaka 18 na 19 ingawa wenye asili ya kisomali au kiarabu na waliishi mjini Minnesota. Mshukiwa mwingine alikuwa mwanamnke Muingereza ambaye inasemekana alikuwa amefanya vitendo vingi vya aina hii kwa niaba ya Al Shabaab.

Shirika la Red Cross limeambia BBC kuwa watu 63 wangali hawajulikani waliko.


Wanajeshi wa Kenya katika juhudi za kuokoa mateka na kukomboa jengo la Westgate Haijulikani idadi ya wanamgambo waliokuwa ndani ya jengo hilo , lakini maafisa wa usalama wamesema kuwa wanamgambo watatu wameuawa.

Kundi la kigaidi la al-Shabab limekiri kutekeleza mauaji hayo, kulipiza kisasi hatua ya Kenya kujihusisha kijeshi nchini Somalia.

Operesheni hiyo iliendelea usiku kucha ingawa kwa mujibu wa waziri wa usalama wa Kenya, ilikuwa katika mkondo wake wa mwisho.

"magaidi hawa huenda wanakimbia na kujificha katika sehemu mbali mbali za jengo hilo lakini ghorofa zote za jengo hilo zimedhibitiwa na majeshi,'' alisema Ole Lenku

Aliongeza kuwa mateka wote walifanikiwa kuokolewa.

Jumatatu jioni moshi mkubwa ulionekana ukifuka kutoka kwenye jengo la Westgate ukiambatana na moto mkubwa. Moto huo unasemekana uliwashwa na wanamgambo hao ili kutatiza vikosi vya usalama katika juhudi zao za kutaka kukomboa jengo hilo.